TOTO AFRICANS YAREJEA KILELENI LIGI SOKA DARAJA LA KWANZA TANZANIA BARA ;YAIZAMISHA JKT OLJORO 3-1

Klabu ya soka ya Toto Africans imefanikiwa kurejea kileleni mwa kundi B la ligi soka daraja la kwanza baada ya hapo jana kuizamisha JKT Oljoro ya mkoani Arusha kwa mabao 3-1 kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza

Toto Africans
Kocha mkuu wa Toto Africans John Tegete akitoa maelekezo
 kwa wachezaji wake wakati wa mapumziko hapo jana
Wana-Kishamapanda walianza kuzifumania nyavu za wapinzani kunako dakika ya 19 kwa  bao la penati lililofungwa na Emmanuel Swita  ambaye shuti lake lilimshinda mlinda mlango Amani Simba na kutinga nyavuni
Penati hiyo ilitolewa baada ya nyota wa mchezo wa jana kwa upande wa Toto,Hamim Abdul Karim kufanyiwa madhambi kwenye eneo la hatari na mlinzi wa  JKT Oljoro Yusuph Machogote
JKT Oljoro baada ya kufungwa bao hilo iliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Toto Africans na katika  dakika  28 ilifanikiwa kusawazisha bao kwa njia ya penati kupitia kwa Swalehe Hussein baada ya Ally Ahmed kuangushwa kwenye eneo la hatari na Miraji Maka
Toto Africans ilifunga bao la pili dakika ya 40 kupitia kwa Hamim Abdul Karim aliyefunga kwa shuti kali kufuatia majalo nzuri kutoka winga ya kulia iliyopigwa na Severine Constantine
Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika,Toto Africans ilikuwa mbele kwa mabao 2-1
Nyota wa mchezo wa jana kwa upande wa Toto Africans,Hamim Abdul  Karim katika dakika ya 68 aliifungia Toto bao la tatu baada ya majalo nzuri kutoka winga ya kushoto iliyopigwa na kiungo mkongwe Emmanuel Swita
Hadi filimbi ya mwisho ya mchezo huo inapulizwa,Toto Africans iliondoka na ushindi wa pointi zote tatu na hivyo kuongoza ligi daraja la kwanza kwa kundi B baada ya kufikisha alama 19 katika michezo tisa huku Mwadui FC ya Shinyanga ikiporomoka hadi nafasi ya pili ikiwa na alama  17 lakini ina michezo minane
Baada ya mchezo wa jana,Kocha mkuu wa Toto Africans John Tegete alisema kuwa amefurahishwa na kiwango ambacho wachezaji  wake walikionyesha hapo jana huku akimwagia sifa nyingi mshambuliaji  Hamim Abdul Karim ambaye alifunga mabao mawili
‘Nimefurahishwa sana na haya matokeo,kama umeangalia vizuri kikosi changu kimeimarika.Nimefanya marekebisho kwenye safu ya ushambuliaji ambapo,Hamim Abdul Karim kwenye michezo iliyopita nilikuwa nikimchezesha kwenye nafasi ya ulinzi lakini leo amecheza kwenye ushambuliaji na kufunga mabao mawili na sasa ana jumla ya mabao manne,ni mchezaji mwenye uwezo wa hali ya juu.Nawaambia wakazi wa Mwanza watarajie kuiona timu yao ikitinga Ligi kuu soka Tanzania Bara msimu ujao na nawaahidi kuwa mchezo wetu ujao wa Jumatano ijayo dhidi ya Geita Gold SC tutaibuka na ushindi mzuri’alisema Tegete
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea hii leo kwa michezo mitano kuchezwa ambapo JKT Kanembwa itaikaribisha Polisi Tabora kwenye uwanja wa Lake Tanganyika,Mwadui FC Shinyanga itakuwa mwenyeji wa vibonde Green Warriors kwenye uwanja wa Mwadui,Wafanyabiashara wa mafuta-Panone  FC  watakua wenyeji wa Geita Gold SC   kwenye uwanja wa Mwadui
Burkina Faso ya Morogoro itakua mgeni wa Rhino Rangers kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora huku Polisi Dodoma watakua mwenyeji wa Polisi Mara

Share on Google Plus

About Unknown

"Is the CEO and Co-Founder of wakuganda in sports blog, dedicated to give you Sport roundups, updates, live scores and all sporting events,"
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment