Shirikisho la soka Tanzania, TFF, limesema linakaribisha wabunifu watakaobuni mwonekano wa jezi mpya za timu ya taifa kwa mechi za nyumbani na ugenini.
Hata hivyo sharti la ubunifu huo lazima uzingatie rangi za bendera ya taifa ambazo ni kijani, njano, nyeusi na bluu.
Wakati
tangazo hili likitolewa na TFF, tayari uongozi mpya chini ya rais wake
Jamal Malinzi umebadili jezi zinazotumiwa katika mechi za timu ya taifa,
Taifa Stars, kutoka zile zilizozoeleka na mashabiki na Watanzania wote
hadi jezi mpya zinazolalamikiwa na mashabiki wengi kuwa hazina mvuto na
hazionyeshi rangi halisi ya bendera ya taifa la Tanzania.
TFF ilipoamua kutumia jezi mpya zinazotumika sasa haikuwashirikisha
wabunifu wa mavazi kuhusu jezi mpya ya timu ya taifa na badala yake
ikaja na jezi ambayo imekuwa ikilalamikiwa na mashabiki kuwa haina mvuto
na haiwakilishi rangi halisi za bendera ya taifa, huenda ndio maana
safari hii wametoa tangazo hilo.
Mbunifu atakayeshinda atapata
zawadi ya shilingi milioni moja za Kitanzania sawa na karibu dola mia
saba za Kimarekani kwa atakayebuni jezi ya kuchezea mechi za nyumbani na
vile vile mshindi atakayebuni jezi za kuchezea mechi za ugenini naye
atapata kiasi kama hicho cha fedha.
Jezi ya sasa ina rangi ya samawati na bluu nyeusi.

0 comments:
Post a Comment